KLABU ya Simba imesema iliamua kumweka benchi mshambuliaji wake raia wa Zambia, Felix Sunzu (pichani), kwenye mechi dhidi ya Villa Squad Jumamosi iliyopita ili awe fiti katika mchezo dhidi ya Azam utakaochezwa Jumamosi ijayo kwenye Dimba la Taifa, Dar es Salaam.
Sunzu hajacheza mchezo wowote wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kutokana na kuwa na maumivu ya kifundo cha mguu aliyoyapata kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Tusker mwezi mmoja uliopita.
Akizungumza na Mguso, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema Sunzu alipona tangu wiki iliyopita lakini waliamua kumtunza kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Azam.
“Sunzu yupo fiti kuwavaa Azam na ndiyo risasi tuliyoiweka benchi kwa ajili ya kumaliza kazi haraka Jumamosi pale Uwanja wa Taifa. Tunatambua ugumu wa mechi hiyo ndiyo maana tukaamua tumpumzishe dhidi ya Villa,” alisema Kamwaga.
Mchezo dhidi ya Azam unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na Azam kuwa katika mwendo mzuri katika ligi kwa sasa huku ikiwa imeshinda mechi zote tatu za mzunguko wa pili na inashika nafasi ya pili nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi mbili.
No comments:
Post a Comment