Tuesday, February 7, 2012

MOHAMMED MWAMEJA AKICHAMBUA "KIWANGO" CHA JUMA KASEJA


KIPA wa zamani wa Simba, Mohammed Mwameja, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha unampa kipa Juma Kaseja, msaada wa kisaikolojia kabla ya mchezo dhidi ya Kiyovu.

Mwameja ambaye aliwahi kuidakia timu hiyo kwa mafanikio makubwa akiwa na sifa ya kuokoa mashuti pamoja na penalti, alisema haridhishwi na kiwango cha Kaseja kwa sasa.

Akizungumza na Mguso, Mwameja alisema Kaseja anatakiwa kutengenezwa kisaikolojia na kimazoezi kabla ya mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Wanyarwanda hao.

 “Kaseja anahitaji msaada wa haraka wa kutengenezwa, kwa sasa inaonekana kama hayupo fiti. Jinsi alivyo siyo Kaseja ninayemfahamu. Nilifanikiwa kumuona wakati wa michuano ya Chalenji, siyo Kaseja yule wa miaka mitatu iliyopita.

“Sijajua tatizo ni nini mpaka amepoteza uwezo wake, nafikiri hata umri unachangia na kucheza mechi nyingi mno ni tatizo,” alisema Mwameja.

Simba inatarajiwa kucheza na Kiyovu kati ya Februari 17 na 19 mwaka huu jijini Kigali na kurudiana kati ya Machi 2 hadi 4 jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment